CONTACT US:

CONTACT US:
Mobile : 0755 484866
EMAIL : socialworkertz@yahoo.com

Thursday, November 17, 2011

Mtoto huyu akifa, sababu ni mil. 3



Mtoto Pascal Tano akiwa na mama yake, Jane Leo, katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili

HII inauma sana, mtoto anaumwa, mzazi amegundua tatizo linalomsumbua lakini fedha ya matibabu hakuna. Wapo wapi waliojaliwa na Mungu kumuokoa malaika huyu wa Mungu?

Mtoto Pascal Tano, mwenye umri wa miaka mitano, ana hali mbaya, amebainika kuwa na matundu kwenye mishipa ya damu lakini badala ya kupata matibabu, kwa sasa yupo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa sababu mama yake hana fedha za kumgharamia.

Jane Leo, mama mzazi wa Pascal aliliambia Uwazi kuwa mwanaye alifanyiwa kipimo cha OGD kwenye Hospitali ya Aga Khan na kubainika kwamba ana matundu katika mshipa wa damu tumboni.

Alisema, baada ya vipimo kubaini hivyo, ilitakiwa achomwe sindano sita ambazo kila moja gharama yake ni shilingi 460,000 pamoja na dawa ya usingizi chupa sita, ambazo zinagharimu shilingi 50,000 kila moja.

“Jumla ya fedha zote zinazohitajika ni shilingi 3,100,000. Hizo fedha nitazipata wapi mimi maskini ya Mungu? Nina mawazo mengi juu ya afya ya mtoto wangu,” alisema Jane.

MTOTO AMETESEKA!
Kwa mujibu wa Jane, Pascal alianza kuugua tangu akiwa na umri wa miezi tisa, hali ambayo ilimlazimu kutembea hospitali mbalimbali kutafuta matibabu.

Jane, mkazi wa Kijiji cha Statike, Wilaya ya Mpanda, Rukwa alisema: “Tatizo lilianza kwa homa za mara kwa mara, tumbo kujaa, kukohoa na kutapika damu. Nilimpeleka Hospitali ya Mpanda lakini hawakugundua ugonjwa. Hali ilizidi kuwa mbaya, akaongezewa damu lita nne lakini wapi.

“Kimsingi aliongezewa damu mara nyingi. Akiwa na miaka mitatu nilimpeleka Hospitali ya Mkoa wa Singida, madaktari wakasema anaumwa kifua kikuu. Tulipewa dawa lakini hazikusaidia. Pamoja na uhaba wa fedha, nilimpeleka Hospitali ya Mkoa wa Tanga akiwa anatapika damu mara kwa mara lakini hatukupata mabadiliko.

“Madaktari wa Tanga walishauri nimpeleke Muhimbili, Agosti 26, mwaka huu nilifika Dar. Moja kwa moja, nikaenda Muhimbili, akapigwa x-ray, ugonjwa haukuonekana. Nikaandikiwa kipimo cha OGD ambacho kilifanyika Aga Khan ndipo lilipobainika tatizo la matundu kwenye mshipa wa damu tumboni.

“Kipindi chote nazunguka mwenyewe kwa sababu mume wangu amebaki Mpanda, anamlea mtoto wetu mdogo mwenye umri wa miaka miwili ambaye anaitwa Januari. Hapa nilipo sina mbele wala nyuma, naomba Watanzania wanisaidie kumpatia matibabu mtoto wangu na Mungu atawalipa.

“Watanzania wasikie kilio changu, wanaoguswa na tatizo la ugonjwa wa mwanangu na kuwa na lengo la kuokoa maisha yake wanisaidie kwa kuwasiliana na mimi. Namba yangu ni 0753-673815 au hata wakiniulizia Muhimbili, watanipata.”

No comments:

Post a Comment