Takwimu mpya za WHO juu ya maambukizi ya vimelea vya H1N1
Dktr Keiji Fukuda, Mkurugenzi Mkuu Mwandamizi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), kwenye mahojiano Alkhamisi na waandishi habari mjini Geneva, alitangaza takwimu mpya juu ya maambukizo ya homa ya mafua ya nguruwe, ambayo kuanzia leo itajulikana rasmi kama homa ya vimelea vya H1N1.
Alisema wagonjwa 236 walisajiliwa rasmi kimataifa kuambukizwa na vimelea vya H1N1, takwimu ambayo Ijumatano ilijumlisha wagonjwa 148. Katika Mexico maabara za uchunguzi wa maradhi zimethibitisha wagonjwa 97 waliuguwa homa ya H1N1 na kusabibisha vifo saba. Idadi ya watu walioambukizwa na homa hiyo inaendelea kuongezeka Mexico ambako maofisa wakaazi wa afya wa WHO, wakijumuika na wahudumia afya wa kizalendo, wanaendelea na uchunguzi wao, kupima maelfu ya sampuli kutoka wagonjwa, zilizokusanywa na idara ya afya. Ijumatano Shirika la WHO lilitangaza kupandisha daraja ya tahadhari ya mripuko wa maambukizo ya homa ya mafua ya nguruwe katika dunia, kutoka daraja ya nne na kuwa daraja ya tano. Daraja ya tano, kwa mujibu wa taarifa za WHO, humaanisha maambukizo ya virusi/vimelea vya homa hutawanywa baina ya wanadamu, hali ambayo ni lazima idhibitiwe kidharura na nchi wanachama, ili kupunguza kasi ya maambukizo, na kudhibiti maradhi yasije yakazusha janga la afya kimataifa. Katika kipindi hiki mataifa huwa yanatarajiwa kukamilisha matayarisho ya huduma za kizalendo kwenye udhibiti wa, kijumla, wa mripuko wa maradhi, ili usije ukaambukiza idadi kubwa ya raia. Wakati wa mfumko wa homa ya mafua ya ndege ulipojiri katika miaka ya 2005-2006, kampuni ya madawa ya Roche ya Uswiss ilifadhilia WHO mamilioni ya vifaa na madawa ya kutumiwa, kwa madhumuni ya kusaidia udhibiti bora wa maradhi kimataifa. Hivi sasa WHO imeanza kugawia madawa kinga dhidi ya homa ya h1n1 kwenye zile nchi masikini muhitaji, ambazo hazimudu kuzinunua dawa hizo, ikijumlisha vile vile taifa la Mexico ambalo ndilo lilioathirika kwa kiwango kikubwa katika kipindi cha hivi sasa.
No comments:
Post a Comment