CONTACT US:

CONTACT US:
Mobile : 0755 484866
EMAIL : socialworkertz@yahoo.com

Tuesday, October 25, 2011

Simulizi ya majonzi jamii ya wakoma, Hombolo, Dodoma


Moja ya nyumba wanamoishi familia yenye matatizo ya ukoma.

Na Richard Manyota
TANGU nianze kusimulia mateso ya jamii ya wenye ukoma nilikuwa nikipokea simu kutoka sehemu mbalimbali, watu wakionesha kugushwa na matatizo hayo.

Hivi karibuni Mchungaji wa Kanisa la Yerusalemu Assemblies Of God, lililopo jijini Dar es Salaam, Tuli Abrahamu Mwaipopo alifunga safari hadi kijijini Hombolo kwa lengo la kujionea mwenyewe juu ya yale aliyokuwa akiyasoma kwenye makala haya.

“Nilipokuwa nikisoma nilidhani mnatia chumvi kunogesha habari zenu, ikabidi niende huko, Oktoba 14 niliwasili kijijini Samaria, nilipofika kila nilikokuwa kinikatiza nilibubujikwa na machozi, sikuwahi kuona maisha ya shida kama wanayoishi wakazi wa Samaria.” Anasema Mchungaji Tuli.

Tuli, anakubaliana nami kuwa niliyokuwa nikiyaandika kwa majuma matatu yana ukweli uliopungua, kwani alinikosoa baadhi ya maelezo kwamba nilishindwa kuandika maneno yanayoendana na hali halisi ya huko.

Anasema, akiwa huko alikutana na watoto, wanawake na watu wenye matatizo mazito na hivyo kutoa mwito kwa wachungaji wenzake huku akiwataja baadhi kwa majina kama mchungaji Getrude Rwakare, Onesmo Ndegi, kuwa msaada wao unahitaji kwa haraka kijijini Samaria.

“Kama kweli tumeletwa duniani kusaidia wenye shida, kutoa huduma za kichungaji, basi lazima tufike Samaria, tuwasaidie wakazi wa huko na kuwatia moyo,” anasema Tuli ambaye yeye katika safari yake hiyo licha ya kutokujiandaa aliwasaidia wakazi wa huko kilo 100 za unga na fedha kidogo.

Nakiri mama Mchungaji Tuli amenisaidia kufikisha ujumbe kwa watumishi wa mungu na kuthibitisha ukweli wa makala haya ambayo leo tunafikia tamati.
Kama mzalendo wa kweli wa nchi hii siwezi kuwa na ziada ya maneno ya kushawishi watu kujitolea kuwasaidia wakoma wa samaria zaidi ya haya niliyoandika kwenye mfululizo wa makala haya.

Wito wangu ni kwamba, kwa yeyote anayegushwa na shida za watu hawa anaweza kujitokeza na kuahidi atasaidia nini?
Gazeti la Uwazi kwa kushirikiana na Taasisi ya LIWILE tutasimamia uratibu wa michango hiyo ambapo tutaoa muongozo baadaye wa namna ya kuwachagia watanzania wenzetu wanateseka huko kijijini Samaria.

Kwa kifupi, kijiji cha Samaria kina zaidi ya Kaya 42, msaada wa haraka unaohitajika huko ni chakula, maji, dawa, nguo, magodoro, vyandarua, vyombo vya kupikia na kulia chakula pamoja na ukarabati wa makazi yao ambapo wengi kati ya wakazi wa eneo hilo wakiwemo watoto wanalala kwenye magofu ambayo ni hatari kwa maisha yao.

Tunatanguliza shukrani zetu za dhati kwa wote watakaochangia harambee ya kuwasaidia wakoma wa Samaria. Kwa wale wanaotaka kupeleka misaada yao moja kwa moja tutawaelekeza. Namba za kupata maelezo ya ziada ni 0714-895555, 0655-017116. Shukrani kwa Gazeti la Uwazi na Mradi wa LIWILE.

No comments:

Post a Comment