Ni unyama wa aina yake umefanyika jijini Dar es Salaam baada ya wanaume 16 kudaiwa kumbaka na kumlawiti mtoto wa miaka 14 mfululizo na kumuacha akiwa hajitambui.
Hali ya mtoto huyo inadaiwa kuwa mbaya baada ya sehemu zake za siri mbele na nyuma kuharibika na kusababisha kutokwa na damu na usaha muda wote.
NIPASHE Jumapili ilifika nyumbani anakoishi mtoto huyo na kumkuta akiwa amelala chini kutokana na maumivu anayoyapata baada ya kufanyiwa unyama huo.
Akiongea na mwandishi wa habari hizii kwa taabu, alisema tukio hilo alikumbana nalo Agosti 31, mwaka huu majira ya saa 5 usiku jirani kabisa na makazi anayoishi na bibi yake.
Akisimulia mkasa mzima alisema kwamba siku ya tukio majira ya saa 3 usiku alikuja mwalimu wake anayemfundisha maigizo nyumbani kwao na kumtaka waende nyumbani kwake.
Alisema wakati huo alikuwa pamoja na rafiki yake, hivyo alimuomba waongozane wote hadi nyumbani kwa mwalimu wake huyo, hapo ndipo safari yao ilipoanza wakiwa watatu yaani yeye, rafiki yake na mwalimu wake wa mazoezi.
Binti huyo alisema hakuwa na wasiwasi na safari hiyo kutokana na heshima ya mwalimu wake. Walipofika nyumbani kwake waliongea kidogo na baada ya kuona muda unazidi kwenda alimuomba mwalimu wake awarudishe nyumbani kwao ili wakalale.
Alisema mwalimu wake alikubali kuwasindikiza hadi barabarani. Walipofika sehemu waliyokubaliana, mwalimu huyo aliwakabidhi kwa kijana mwingine wa kiume akieleza ataweza kuwafikisha nyumbani kwao salama.
“Nilimwambia yule kijana hakunifuata nyumbani ila namtambua yeye, lakini alisisitiza kuishia hapo na kutupa yule mwenzake ili atupeleke nyumbani," alisema.
Wakati wakitembea kuelekea nyumbani kwao, njiani yule kijana aliwataka wachukue mawe kwa sababu anajua mbele watakumbana na matatizo, hata hivyo hakuyataja.
Kabla hawajachukua mawe hayo, kundi la vijana wa kiume wanaokadiriwa kuwa na umri wa miaka 18-28 liliwavamia na kuanza kuwavuta na kuwatishia kuwakata kwa mapanga.
Katika msukosuko huo, rafiki yake alifanikiwa kukimbia na kumuacha yeye akiwa amebebwa na watu hao na kumpeleka kwenye kichaka kilichokuwa karibu na mwembe uliokuwa jirani na barabara.
Alisema alipofikishwa hapo, watu hao walimvua nguo zote na kuanza kumbaka kwa zamu. Kitendo hicho kiliendelea kwa muda hadi hapo mwendesha pikipiki alipokuja kuwashtua na kuamua kumchukua na kumpeleka kwenye gofu la nyumba ambayo haijakamilika na kisha wakaendelea na unyama wao.
Kutokana na maumivu makali aliyokuwa akipata, binti huyo alijaribu kupiga kelele lakini alishindwa kutokana na kuzibwa mdomo na macho.
Cha kusikitisha, watu hao walijipanga foleni na kuendelea kumuingilia kwa zamu watu wawili wawili.
“Nililia sana na mwishowe sikuweza tena kutoa sauti kutokana na maumivu makali, waliniingilia kwa ukatili mkubwa huku wengine wakiniwekea mapanga kichwani wakinitaka niache kupiga kelele ama sivyo watanikata kichwa,” alisema.
ANUSURIKA KUINGIZWA KISIMA CHA MAJI
Baada ya kuona binti huyo anaishiwa nguvu watu hao waliamua kumchukua hadi kwenye kisima cha maji kwa nia ya kumtumbukiza ili afe na maji kwa kupoteza ushahidi.
Wakati wanajadili mpango huo kulitokea kutoelewana kati yao ambapo mmoja wao alipinga vikali hatua hiyo kwa kuwaambia wasifanye kitu hicho kwani tayari haja zao zimeshakwisha.
Lakini watu wengine hawakukubaliana na kauli ya mwenzao na kuanza kusukumana huku wengine waliamua kumchukua binti huyo ili kwenda kutimiza lengo lao.
Alisema, walipofika kwenye eneo la kisima walimsimamisha pembeni ya kisima hicho huku wenyewe wakiendelea kulumbana, ndipo ghafla alitokea mmoja akamsukuma ili aingie kisimani. Wakati akipepesuka kuelekea ndani ya kisima mwenzao aliyekuwa akipinga kitendo hicho alimuwahi na kumsukuma upande mwingine na kuanguka chini nje kidogo ya kisima.
Baada ya kuona mwenzao amekuwa mkali kuhusu jambo hilo, wote waliondoka eneo hilo na kuwaacha wawili.
"Niliogopa sana baada ya kuona mtu aliyenifanyia unyama ananitetea na kubaki wawili tu pale, nilijua anataka kuendelea kunibaka lakini alinisihi nisiogope ataniokoa," alisema.
Mtu huyo alimchukua toka pale kisimani na kumpeleka hadi kwenye chumba cha rafiki yake kwa ajili ya kumuhifadhi, lakini huko walikutana na wale watu wengine waliombaka kitu ambacho hawakuweza kulala baada ya watu hao kukataa.
Hata hivyo hawakukata tamaa ilibidi kutembea usiku majira ya saa 8:00 usiku hadi kwa rafiki yake mwingine ambapo huko walifanikiwa kulala hadi asubuhi alipopata nafasi ya kuondoka hadi nyumbani kwao na kutoa taarifa.
Kwa mujibu wa maelezo ya mama yake mzazi (jina linahifadhiwa) mara baada ya tukio hilo alichukua hatua ya kumpeleka Hospitali ya Temeke, huko alifanyiwa vipimo na kupewa dawa, lakini walishindwa kuendelea na matibabu kwa kukosa pesa.
Alisema toka siku aliyopatwa na tukio hadi leo anampatia vidonge vya kutuliza maumivu baada kutokuwa na uwezo wa kumudu gharama za matibabu.
“Tumeshindwa kupata pesa zinazohitajika hadi sasa, nampa tu panadol ili kutuliza maumivu, hali ya mwanangu ni mbaya muda wote anatokwa na damu na usaha sehemu zote za siri,” alisema.
Hata hivyo kutokana na maimivu hayo, binti huyo hawezi kutembea kama kawaida na badala yake muda wote amekuwa akilala.
Mama huyo anasema mara baada ya tukio hilo kujulikana waliamua kwenda katika kituo cha Polisi cha Nzasa kwa ajili ya kufungua kesi pamoja na watuhumiwa kukamatwa, hata hivyo walikabiliana na vikwazo baada ya mmoja wa polisi wa kituo hicho aliyekuwa zamu kudai apatiwe pesa ndipo afanye kazi hiyo.
Alisema kutokana na kikwazo hicho waliamua kwenda kituo cha Polisi Mbagala Kizuiani, ambapo huko waliwarudisha tena kituo cha Nzasa na kuwaeleza watawasiliana ili wapewe msaada.
Hata hivyo, waliporudi huko walipewa msaada shingo upande kitu ambacho kilisababisha mtu waliyemkamata kwa tuhuma hizo kutoroka akiwa kwenye mikono yao.
Alisema licha ya kuwakamata watuhumiwa hao kitu cha kusikitisha amesikia watuhimiwa wote wameachiliwa kwa dhamana na sasa wapo mitaani wakitembea.
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Temeke, David Misime alipopigiwa simu kutakiwa kuelezea tukio hilo, alisema tayari jeshi lake limewakamata watu watatu wakituhumiwa na tukio hilo.
Alisema kwa ujumla binti huyo amebakwa na watu 10 kwenye tukio hilo lilotokea majira ya kati ya saa 5:00-6:00 usiku,
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
ooops! hiyo mbaya sana! du! matatizo kama hayo ni udhihirisho tu kwamba dunia imeisha na hivi karibuni Mungu atasimama kuihukumu Dunia, our voices should be louder and louder as you are doing in this blog, i commend you greatly for what you have started in this blog to agitate and raise awareness of social issues,
ReplyDeleteformer Lecture at the institute of Social work, keep it up, good work i have liked what you are doing God bless you! visit my public blog at http://www.tenaimeandikwa.blogspot.com