CONTACT US:

CONTACT US:
Mobile : 0755 484866
EMAIL : socialworkertz@yahoo.com

Wednesday, October 12, 2011

HAYATI JK ALIVIPIGA VITA LEO VINAPIGIWA MAKOFI


Tarehe 14-10-1999, nuru na nyota ya mwanzilishi wa taifa la Tanzania, kipenzi, mwanasiasa mahiri, baba wa taifa na mwanafalsafa wa Tanzania na ulimwengu ilizima ghafla na kukamilisha safari yake ya miaka 77 hapa duniani. Tanzania na baadhi ya pande za dunia wanamkumbuka kila ikifika tarehe 14-10 ya kila mwaka ili kutafakari na kuyaenzi yale yote mema aliyo ya asisi na kuyasimamia. Nikiungana na watanzania na ulimwengu kutafakari mambo mengi ya msingi aliyo aanzisha na kuyasimamia Mwl J.K Nyerere katika hayo nadiriki kusema HAYATI JK ALIVIPIGA VITA LEO VINAPIGIWA MAKOFI.
Hayati Nyerere alipigana kufa na kupona mpaka umauti unamkuta na umaskini, ujinga, maradhi, ukabila, udini , ujimbo na hata umimi. Hivi ni baadhi ya vitu alivyopigana navyo mpaka umauti unamkuta lakini leo vinaendelezwa na wale ambao hayati JK aliwaamini na ndio maana nadiriki kusema vinapigiwa makofi. Ukabila sasa Tanzania unakuwa kwa kasi na viongozi hawachukui hatua madhubuti na wengine wanashiriki kuendeleza. Zamani watanzania tulikuwa hatuna utamaduni wa kuulizana au kutaka kufahamu mtu ni wa kabila gani au anatokea wapi? Leo ni kawaida sana unapokutana na watu au kutambulishwa sehemu mbele za watu kuulizwa we ni kabila gani?au unatokea wapi/mwenyeji wa wapi?au kama ni wa kabila lile la mtambulishaji hudiriki kusema huyu ni wa kwetu hivyo ni mwenzetu,ndugu yetu. Kwenye vyuo vikuu na vyuo vya elimu ya juu kunako aminika kuna wasomi vioo vya jamii wenye uwezo wa hali ya juu wa kuchambua mambo, wanaojua athari za ukabila huko kuna jumuiya na taasisi za kikanda, kimkoa, wilaya na hata jimbo wasomi hawa nao wanadiriki kupigia makofi ukabila na upande mwingine wanasimama kusema wanataka kusimamia yale aliyoyaanzisha Nyerere huku si kupigia makofi aliyopiga vita hayati JK? Nako mitaani tunako ishi ni kawaida sana siku hizi kuona jumuiya kama hizi zilizopo katika vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu eti lengo likiwa ni kusaidiana katika sherehe na misiba, kufahamiana na kuweza kupanga mikakati ya kusaidia maendeleo ya kwao asilia, mbaya zaidi viongozi wa kitaifa ndio wanakuwa walezi wa jumuiya hizi na vyama hivi ambavyo ukivitazama kwa kina ni kuendeleza ukablia, ukanda na hata udini, kama kiongozi wa kitafia anakuwa mlezi wa jumuiya ya kikanda au kikabila huku si kupigia makofi aliyoyapiga vita hayati JK?
Siku hizi kuna asasi au mashirika mabayo yamesajiliwa na utangulizi wake unatamka wazi malengo yake ni kusaidia watu wa kabila fulani na au sehemu fulani ya nchi na bado msajili wa vya vya kiraia anavisajili huku si kupigia makofi?kwani misaada haiwezi kutolewa mpaka uwe kwa watu wa kabila husika la watoaji msaada?hivi hatuwezi kizikana, kusaidiana na kufahamiana mpaka tutumie ukabila na ukanda wetu?uko wapi utanzania wetu?nani kaangusha ile nguzo na ufahari wa utanzania wetu?
Dhambi ya ukabila inaitafuna Tanzania sasa mpaka kwenye vyama vya siasa, tumeshasikia chama fulani uteuzi wa wabunge wa viti maalumu ulikuwa wa upenedeleo zaidi kwa watu wa kabila la mwenyekiti wake, kuna chama kingine kilivuma eti ni cha watu wa imani fulani ya dini. Hivi karibuni katika uchaguzi mdogo wa jimbo moja kuna chama kilimpleleka kiongozi mmoja wa kitaifa eti kwa kuwa ni bingwa wa kuzungumza lugha ya kabila la wanacnhi husika na ilishangiliwa na kuripotiwa na magazeti kwa mbwembwe zote huku si ndio kupigia makofi?Mbaya zaidi ukabila unagusa mpaka idara nyeti za serikali zinazogusa maslahi ya taifa, kuna taasisi moja kubwa nchini ilidaiwa kuwa nawatumishi wa kabila fulani wakati huo waziri wa idara hiyo akiwa ni wa kabila hilo, hivi karibuni tumesikika eti kuna wizara moja kiongozi mmoja wa utumishi wa umma anashinikiza viongozi wa juu wa wizara hiyo lazima wawe wa kabila lake. Sasa kama vyama vya siasa vinavyotarajiwa kukabidhiwa dhamana ya taifa hili wanahusudu ukabila na udini taifa hili litabaki salama? Waziri mwenye dhamana ya taifa anaendeleza au anashindwa kukemea ukabila katika taasisis yeneye maslahi ya kitaifa si ndio kupigia makofi huko?kama kiongozi wa utumishi wa umma analazimisha viongozi wa wizara nyeti wawe wa kabila lake na viongozi wakuu wa taifa hawachukia hatua huku si kupigia makofi?
Sio ukabila na udini tu bali hata umimi na usisi unalitafuna taifa letu la Tanzania, siku hizi tenda kubwa zote za serikalini viongozi wana zinachukuwa wao kupitia kampuni zao au za washirika wao tena kwa gharama mara mbili au zaidi ya gharama husika na kuongeza ombwe la kipato baina ya mwananchi mmoja mmoja, matajiri na maskini na ni kawaida sana kuona mtu kabla hajawa kiongozi alikuwa maskini au wa kipato cha wastani ila baada ya miaka kadhaa katika uongozi anakuwa tajiri wa kupindukia, mbona miaka 21 ya hayati JK madarakani na bado alikufa maskini?leo miaka 10 ya viongozi wa leo wanageuka mabilionea kama si kupigia makofi umimi na usisi alipiga vita hayati JK ni nini huu? Ukienda kwenye ajira wahitimu wengi wa vyuo vikuu wanahangaika kupata ajira lakini kuna wengine wanapata kirahisi au kilaini kwa kuwa wana wafahamu viongozi wa idara husika au wana jamaa na ndugu wenye ushawishi mkubwa kwa viongozi husika. Siku hizi ajira zimekuwa si kwa vigezo vya sifa, uwezo wa kitaaluma na uzoefu bali inategemeana unamfahamu nani?nani kakupeleka pale?huku si kupigia makofi?huu si ndio ubinafsi, umimi na usisi?
Siku hizi ukimaliza muda wako wa utumishi uliotukuka na hauna mali jamii iankucheka na kukushangaa imekuaje umekuwa maskini, siku hizi utumishi ulitukuka hauko tena umimi na ubinafsi unaolazimishwa na jamii umejaa katika mioyo yetu, kila mtu anafanya kazi ili apate mali yake , apate vyake ili ukifika wakati wa kupumzika jamii isimcheke. Tunapinga ufisadi kwa nguvu zote ila mafisadiila fedha zao na michango yao ya fedha zao chafu tunazitaka, ndio fedha zinazotumika kupata viongozi na kujenga nyumba za ibada au ndio ule usemi wa Kiswahili baniani mbaya kiatu chake dawa?ila huku si ndio kupigia makofi
Nadiriki kutamka Hayati JK alivipiga vita, leo vinapigiwa makofi tena walio wengi wanaoendekeza, wanaofanya au waliofanya yale aliyoyapiga vita hayati JK ni wale ambao aliwaamini, waliomsadia katika mapambano lakini leo wamemsaliti na kugeukia kule alikokupiga vita. Ila bila haya wala soni wakipanda majukwaani wanajifanya bado wanaamini na kusimamia aliyoyaanzisha, leo angerudi na kuwaona sijui angefanya nini kuwaona wale wanaodai kumeenzi kwa kufanya matamasha na makongamano makubwa yenye kuchukua fedha nyingi ya kumuenzi lakini ukweli wa mambo katika maisha wanafanya au wanashiriki kwa njia moja au nyingine kuendeleza aliyoyapiga vita mpaka umauti unamkuta

Mwandishi wa makala hii ni


MR, BARAKA MWAGO.
Afisa Ustawi Wajamii

No comments:

Post a Comment